Genesis 39

Yusufu Na Mke Wa Potifa

1Wakati huu Yusufu alikuwa amechukuliwa mpaka Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa aliyekuwa mmojawapo wa maafisa wa Farao, mkuu wa ulinzi, akamnunua Yusufu kutoka kwa Waishmaeli waliomleta Misri.

2Bwana alikuwa pamoja na Yusufu, naye akastawi, Yusufu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri. 3Potifa alipoona kuwa Bwana alikuwa pamoja na Yusufu na kwamba Bwana alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, 4Yusufu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. 5Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yusufu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo, Bwana aliibariki nyumba ya Mmisri huyo kwa sababu ya Yusufu. Baraka ya Bwana ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. 6Kwa hiyo Potifa akamwachia Yusufu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yusufu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu chochote isipokuwa chakula alichokula.

Yusufu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia;
7baada ya kitambo mke wa Potifa akamtamani Yusufu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!”

8Lakini Yusufu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa katika uongozi, bwana wangu hahusiki na kitu chochote katika nyumba hii, kila kitu alicho nacho amenikabidhi. 9Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu chochote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?” 10Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yusufu siku baada ya siku, Yusufu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye.

11Siku moja Yusufu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwepo na mfanyakazi yeyote ndani ya nyumba. 12Mke wa Potifa akashika vazi Yusufu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yusufu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.

13Yule mwanamke alipoona kwamba Yusufu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba, 14akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga kelele. 15Aliposikia kelele za kuomba msaada, akaacha vazi lake kando yangu akakimbilia nje.”

16Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye mpaka Potifa aliporudi nyumbani. 17Ndipo akamweleza kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa wa Kiebrania uliyetuletea alinijia ili kunidhihaki. 18Lakini mara nilipopiga kelele kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu akakimbia nje ya nyumba.”

19Potifa aliposikia kisa hiki mkewe alichomweleza, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda.” Hasira ya Potifa ikawaka. 20Potifa akamchukua Yusufu na kumweka gerezani, mahali ambapo wahalifu wa mfalme walikuwa wamefungwa.

Lakini wakati Yusufu alipokuwa huko gerezani,
21Bwana alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza. 22Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yusufu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani. 23Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu chochote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yusufu, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja na Yusufu akimfanikisha kwa kila alichofanya.
Copyright information for SwhKC